Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Syria inawakatisha wengi tamaa na maelfu kukimbilia Ulaya- UNHCR

Hali Syria inawakatisha wengi tamaa na maelfu kukimbilia Ulaya- UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limesema kuwa hali inayozidi kuzorota ndani mwa Syria na nchi jirani inawashinikiza malefu ya Wasyria kuhatarisha kukata tamaa na kufanya safari hatarishi kukimbilia Ulaya. Priscilla Lecomte na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Priscilla)

UNHCR imesema wakati mzozo wa Syria ukiwa katika mwaka wa tano bila dalili za suluhu la kisiasa, wengi wamepoteza matumaini.

UNHCR imesema raia wa Syria ambao sasa wamepoteza vitega riziki vyao, wanakabiliwa na changamoto kubwa kupata usalama katika nchi jirani. Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR, Geneva..

“Ndani ya Syria, miezi michache iliyopita imekuwa katili. Kwa wakimbizi zaidi ya milioni 4 wanaoishi katika nchi jirani, na ambao wengi wao wanaishi nje ya kambi rasmi, matumaini yanazidi kutoweka, huku wakiendelea kukabiliwa na umaskini uliokithiri. Kwa mfano, utafiti uliofanywa karibuni Jordan na Lebanon umeonyesha kuwa wakimbizi wamo hatarini zaidi wakati ufadhili ukiwa haba kwa programu za kuwasaidia.”

Kutokana na idadi kubwa mno ya wakimbizi, usaidizi haba wa kimataifa na wasiwasi kuhusu usalama, nchi hizo jirani za Syria zimechukua hatua za kuzuia wakimbizi zaidi kuingia.