Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yapitia upya mpango wa nyuklia wa Iran, huko DPRK ujenzi unaendelea

IAEA yapitia upya mpango wa nyuklia wa Iran, huko DPRK ujenzi unaendelea

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA Yukiya Amano amesema ofisi yake inapitia upya taarifa iliyotolewa na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Amesema hayo wakati akituhutubia kikao cha bodi ya magavana wa shirika hilo mjini Vienna, Austria akiongeza kuwa mapitio hayo yatahusisha pia kuthibitisha na kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran kufuatia makubaliano kati ya nchi hiyo na wasuluhishi wa kimataifa mwezi wa Julai inayopatia fursa zaidi IAEA kuingia maeneo yenye mitambo.

(Sauti ya Amano)

“Utekelezaji wa itifaki ya ziada ni sharti muhimu kwa shirika kuweza hakikisho sahihi kuhusu kutokuwepo kwa dutu za nyuklia ambazo hazijawekwa bayana na Iran. Nchi hiyo pia imekubali kutekeleza mikakati ya uwazi zaidi ambayo itasaidia shirika kuwa na uelewa bora zaidi wa mpango wa nyuklia wa Iran."

Kuhusu Jamhuri kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK, Bwana Amano amesema shirika lake lina ukomo katika uelewa wa mpango wake wa nyuklia na kwamba picha za setilaiti zimeonyesha ukarabati na ujenzi katika mtambo wa nyuklia wa Yongbyon.

Amesema picha hizo ni kithibitisho cha kauli za DPRK kuwa inaendeleza uwezo wake wa kinyuklia.