Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la uhamiaji Ulaya, Ban azungumza na viongozi kwa simu

Janga la uhamiaji Ulaya, Ban azungumza na viongozi kwa simu

Wakati janga la wahamiaji wanaosaka hifadhi Ulaya likichukua sura mpya kila uchao, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameendelea na jitihada za mashauriano na viongozi wa bara hilo ili kuweza kupata suluhu.

Miongoni mwa harakati hizo ni mazungumoz yake kwa njia ya simu na viongozi hao ambapo amewasihi wawe sauti ya wale wanaohitahi hifadhi na hivyo wachukue hatua za haraka kuwasaidia.

Amesema anatambua changamoto kubwa ambazo wimbi hilo la uhamiaji linaleta barani Ulaya na kwa nchi husika lakini amesihi wachukue hatua.

Ban amewapongeza kwa kupaza sauti zao dhidi ya ongezeko la chuki dhidi ya wageni kwa wahamiaji hao, ubaguzi na hata ukatili dhidi ya wahamiaji na wakimbizi barani Ulaya.

Amesema ni matumaini yake kuwa hali hiyo itapatiwa suluhu bila kuchelewa.

Katibu Mkuu amewahakikishia viongozi hao wa Ulaya kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea na jitihada za kuunga mkono bara hilo katika hatua kama vile kupata hifadhi kwa kuzingatia haki za binadamu na viwango vya kibinadamu.