Skip to main content

Mlipuko wa Polio Ukraine, UNICEF, WHO yachukua hatua

Mlipuko wa Polio Ukraine, UNICEF, WHO yachukua hatua

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la afya, WHO yametoa wito kwa wazazi nchini Ukraine kuwapeleka watoto wao kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kuripotiwa nchini humo.

Wito huo umetolewa wakati huu ambapo harakati za kusambaza chanjo zinaendelea baada ya wagonjwa wawili kuthibitishwa katika maabara ya WHO, wagonjwa ambao ni watoto wenye umri wa miezi 10 na mwingine miaka minne.

Watoto hao walipooza baada ya kuambukizwa kirusi cha polio na imeelezwa kuwa hawakuwa wamepatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine Giovanna Barberis amesema njia pekee ya kuwalinda watoto ni kuwapatia chanjo katika nchi hiyo ambayo uelewa wa jamii juu ya hatari za ugonjwa huo unaosababisha kupooza bado ni mdogo.

Kwa mujibu wa utafiti wa UNICEF na WHO, ni asilimia 18 tu ya akina mama nchini Ukraine ambao wanadhani kuwa Polio ni ugonjwa hatari ilhali asilimia 27 wanatambua inaweza kusababisha kupooza.