Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ruzuku ya serikali kwa wakulima huenda ikaongeza uharibifu wa misitu- UNEP

Ruzuku ya serikali kwa wakulima huenda ikaongeza uharibifu wa misitu- UNEP

Ripoti mpya ya Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, imesema kuwa ruzuku ya serikali kwa wakulima, ambayo inakadiriwa kuwa dola bilioni 200 kila mwaka, huchangia pakubwa katika uharibifu wa misitu kote duniani, huku watunga sera wakiwa hawatambui athari zake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takriban asilimia 80 ya uharibifu wa misitu duniani hutokana moja kwa moja na shughuli za kilimo.

Ripoti hiyo inatizama jinsi ya kuoanisha ruzuku za serikali na vyombo vingine vya fedha, kwa dhamira ya kupunguza uchafuzi utokanao na ukataji miti na uharibifu wa misitu katika nchi zinazoendelea.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Achim Steiner, amesema madhara ya ruzuku kwa misitu mara nyingi hutokana na sera potofu na zilizopitwa na wakati.