Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za wananchi, Rais wa Guatemala ajiuzulu, Ban atoa tamko

Harakati za wananchi, Rais wa Guatemala ajiuzulu, Ban atoa tamko

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anafahamu uamuzi wa kujiuzulu wa Rais wa Guatemala Otto Pérez Molina akisema anaamini kuwa mamlaka husika zitazingatia katiba na kuhakikisha demokrasia katika kipindi cha mpito.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu akitoa wito kwa wananchi wa Guatemala kuhakikisha chaguzi za Jumapili hii ikiwemo wa Rais zinafanyika katika mazingira ya amani.

Katibu Mkuu amesema anafahamu matamanio ya wananchi ya kuondokana na rushwa na ukwepaji sheria huku akitoa wito kufanyika kwa marekebisho ya kisiasa na kisheria.

Amekaribisha harakati za wananchi wa Guatemala za kushiriki katika kuimarisha mfumo wa siasa wa nchi yao huku akitoa wito kwa mamlaka na sekta zote za jamii kuimarisha taasisi na utawala wa kisheria nchini humo.