Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Project Everyone kwa siku Saba kufikia watu Bilioni Saba kuhusu SDGs

Project Everyone kwa siku Saba kufikia watu Bilioni Saba kuhusu SDGs

Mtunzi wa filamu mashuhuri duniani, Richard Curtis leo kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa wametangaza mkakati wa kampeni ya siku saba ya kufikisha kwa wakazi Bilioni Saba wa dunia hii malengo 17 ya maendeleo ya endelevu, SDGs yatakayozinduliwa baadaye mwaka huu.

Shughuli hiyo imefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani mbele ya waandishi wa habari ikibeba jina la Project Everyone, shughuli ambayo ilitanguliwa na onyesho la filamu fupi kuhusu muktadha wa kampeni hiyo.

Filamu hii inaonyesha mafanikio yaliyopatikana kupitia malengo ya maendeleo ya milenia ikiwemo kupunguza kwa asilimia 50 umaskini duniani na hivyo filamu inahoji kwa nini kuishia kati? Hata mabingwa kama Usain Bolt hawezi kuishia mita 50 badala yake anakamilisha mita 100 hivyo Project Everyone inataka kukamilisha kazi kupitia malengo endelevu, SDGs.

Akizungumza kwenye tukio hilo Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu SDGs Amina Mohammed amesema..

(Sauti ya Amina)

Inahusu kile ambacho tunataka kiwe matokeo. Tunataka watu wayafahamu, wayakubali kwa njia ambazo watayapigia chepuo, lakini pia kwa njia ambazo watawekeza kwenye ajenda 2030. Tumehakikisha na tunahakikisha kuna tofauti ili rasilimali zinazohitajika zinapatikana.”

Awali akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa Mtunzi huyo wa filamu Curtis amesema ni vyema kila mtu akaelewa fika malengo ya maendeleo endelevu kwa kuwa usichokifahamu huwezi kukijali kwa hiyo..

(Sauti ya Curtis)

“Tunajaribu kuhakikisha malengo yanamfikia kila mtu. Kwa hiyo tulichofanya tumechambua mbinu za kuwafikia watu. Facebook ilikuwa inawafikia watu. Tutajaribu kuweka vitu vya kufurahisha kufikia watu kwenye Facebook. Asilimia 92 ya watu duniani bado wanasikiliza Radio, tutatumia kwenye wiki hiyo. Senema, mambo makubwa tumezungumza na kampuni ya matangazo ya SAWA kuweka matangazo kwenye kumbi za senema ili kujaribu kufikia nchi nyingi duniani. Tutajaribu kufikia shule. Kwa hiyo tunachozindua leo ni kiashiria cha rasilimali tutakazotumia.”

Kampeni hiyo ya siku Saba itaanza tarehe 25 mwezi huu wa Septemba hadi tarehe Mosi Oktoba 2015