Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haitoshi kushtushwa na picha za maiti za watoto wakimbizi- UNICEF

Haitoshi kushtushwa na picha za maiti za watoto wakimbizi- UNICEF

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhudumia watoto, UNICEF, Anthony Lake, amesema haitoshi kwa ulimwengu kushtushwa na picha za kuvunja moyo za miili ya watoto iliyosukumwa na mawimbi hadi kwenye mwambao wa Ulaya, au zile za wakimbizi waliofariki dunia kwenye malori na zile za watoto kuvushwa mipaka ya nyaya na wazazi wao waliokata tamaa.

Mkuu huyo wa UNICEF amesema wakati mzozo wa wakimbizi Ulaya ukizidi kuongezeka, picha hizo za kushtua hazitakuwa za mwisho kwenye runinga, magazetini au mitandao ya kijamii.

Bwana Lake ameongeza kuwa mshtuko huo unapaswa kwenda sanjari na vitendo, kwani hatma ya watoto hao haitegemei chaguo lao, wala hawaidhibiti.

Aidha, amesema watoto hao wanahitaji ulinzi, na wana haki ya kulindwa, akipendekeza hatua kadhaa za kuchukuliwa ili kuwalinda watoto hao, kama vile kutoa huduma muhimu wakati wote, zikiwemo za afya, chakula, usaidizi wa kihisia, elimu, na makazi kwa wahamiaji na wakimbizi, pamoja na kupeleka idadi ya kutosha ya wataalam wa maslahi ya watoto ili wawasaidie watoto hao na famlia zao.