Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yataka huduma bora kwa watoto wakati Liberia ikitangaza kumalizika Ebola

UNICEF yataka huduma bora kwa watoto wakati Liberia ikitangaza kumalizika Ebola

Kwingineko, Shirika hilo la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, limekaribisha leo tangazo kuwa Liberia imekomesha maambukizi ya Ebola, na kuelezea matumaini yake kwamba nchi hiyo sasa itaweza kujikita katika kujikwamua kutokana na mlipuko wa homa hiyo, ambao umeathiri vibaya maisha ya maelfu ya watoto na jamii zao. Taarifa kamili na Joseph Msami.

(Taarifa ya Msami)

Mwakilishi wa UNICEF nchini Liberia, Sheldon Yett, amesema kuwa miezi 17 iliyopita imekuwa kipindi cha kutisha kwa watoto na familia zao, akiongeza kuwa hata kabla ya mlipuko wa Ebola, watoto wa Liberia walikumbwa na uhaba wa huduma bora za afya, elimu na huduma za kijamii.

Ameongeza kuwa sasa kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuboresha huduma hizo na kujiandaa vyema kwa matishio mengine kwa afya.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, zaidi ya watoto 4,500 nchini Liberia ama walimpoteza mzazi mmoja au wote, au mlezi wao kutokana na homa ya Ebola.

Idadi ya watoto walioathiriwa hivi kwa ujumla katika nchi tatu zilizoathiriwa zaidi na Ebola ni 19,300, zikiwemo Guinea na Sierra Leone.