Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asifu China kwa usuluhishi wa mizozo:

Ban asifu China kwa usuluhishi wa mizozo:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyeko ziarani nchini China kushiriki maadhimisho ya miaka 70 ya kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia amekuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Rais  Xi Jinping.

Taarifa ya msemaji wake imesema viongozi hao wawili wamejadili miaka 70 ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa mwishoni mwa vita hivyo ambapo Ban amepongeza China kwa ushiriki wake katika masuala ya kimataifa na mchango wake wa kuokoa maisha ikiwemo ulinzi wa amani na harakati dhidi ya Ebola.

Halikadhalika amezungumzia matarajio yake ya kuonana na Rais Xi baadaye mwezi huu jijini New York, Marekani wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa sanjari na kikao cha ngazi ya juu kuhusu ushirikiano wa nchi za Kusini ulioandaliwa kwa pamoja na serikali ya China.

Ban pia ametoa wito kwa China kuendelea na harakati za kuchocha kasi ya kuelekea mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi baadaye mwaka huu huko Paris Ufaransa na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu yatakayopitishwa baadaye mwezi huu.

Kuhusu ulinzi na amani, Ban amepongeza China kwa dhima yake ya usuluhishi kwenye suala la rasi ya Korea, Sudan Kusini na Iran.