Baraza la Usalama laongeza muda wa vikwazo vya silaha Liberia

2 Septemba 2015

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja wamepitisha azimio la kuongeza muda wa vikwazo kuhusu silaha nchini Liberia kwa miezi tisa.

(Sauti ya Churkin)

Ni Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Septemba, Balozi Vitaly Churkin wa Urusi, akitangaza matokeo ya kura iliyoongeza muda wa vikwazo hivyo vilivyowekwa na azimio nambari 1521 la mwaka 2003, na kufanyiwa marekebisho na maazimio mengine yaliyofuata miaka ya 2006, 2009, 2010 na 2013.

Aidha, Baraza hilo limeamua kuondoa vikwazo vya usafiri na vya fedha vilivyowekwa na azimio 1521 (2003) na 1532 (2004).

Kwa azimio hilo pia, Baraza la Usalama limeamua kuongeza kwa miezi 10, muda wa mamlaka ya jopo la wataalam watakaochunguza na kuandaa ripoti ya mwisho kuhusu utekelezaji na ukiukaji wowote wa vikwazo vya silaha vilivyoongezewa muda leo, vikiwemo vyanzo mbalimbali vya ufadhili wa biashara haramu katika silaha.

Wataalam hao pia wataripoti kuhusu hatua zinazopigwa na serikali ya Liberia katika sekta za usalama na sheria, na uwezo wake kufuatilia ipasavyo na kudhibiti masuala ya silaha na mipaka.

Azimio hilo pia linatoa wito kwa serikali ya Liberia na nchi zote wanachama kushirikiana kikamilifu na jopo la wataalam katika mamlaka yake yote, na kuitolea wito serikali ya Liberia itoe kipaumbele kwa kuridhia hima na kutekeleza sheria inayohusu udhibiti wa silaha, na kupambana na usafirishaji haramu wa silaha.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter