Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Maspika wa mabunge wahitimishwa New York

Mkutano wa Maspika wa mabunge wahitimishwa New York

Mkutano wa nne wa maspika wa mabunge umehitimishwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, huku wito ukitolewa kuwasaidia watu kutimiza ndoto zao.

Wito huo umetolewa na rais wa Muungano wa Kimataifa wa Mabunge, IPU, Saber Chowdhury, wakati wa mkutano huo wenye kauli mbiu, “kujenga ulimwengu wanaotaka watu”, katika muktadha wa malengo mapya ya maendeleo endelevu, SDGs, ambayo yameafikiwa hivi karibuni na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Katika mahiojiano na Radio ya Umoja wa Mataifa, Bwana Chowdhury ameeleza ni kwa nini mkutano wa IPU ni tofauti na mikutano mingine ya Umoja wa Mataifa..

“Hapa ni mahali ambapo serikali huja kutoa ahadi, na sisi tupo hapa, siyo kutoa ahadi, lakini kuhakikisha kuwa ahadi zinazotolewa, zinatimizwa. Kwa hiyo ni kazi ya mabunge. Sisemi kwamba tunatatua matazo ya ulimwengu, lakini tunatoa jukwaa, na ni jukwaa la aina yake. Na jinsi mabunge yatakavyoitikia SDGs, jinsi yatakavyojumuishwa, hatua yatakazochukua, ni muhimu sana kwa ufanisi wake na utekelezaji.”