Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinzi wa Bosco Ntaganda walikuwa ni watoto: ICC

Walinzi wa Bosco Ntaganda walikuwa ni watoto: ICC

Kesi dhidi ya Bosco Ntaganda anayedaiwa kufanya makosa ya uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC kati ya mwaka 2002-2003 imeanza kusikilizwa leo huko The Hague, Uholanzi kwenye makao makuu ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Mbele ya mahakama, Nicole Simpson ambaye ni Mwanasheria mwandamizi wa ofisi ya mwendesha mashtaka, alidai kuwa mshtakiwa akiwa na cheo cha Unaibu mnadhimu mkuu wa kikundi cha UPC alikuwa na mamlaka makubwa juu ya vikosi vyake na yeye binafsi alishiriki uhalifu.

(Sauti ya Nicole)

“Wakati wa shambulizi Novemba 2002 kwenye eneo la Mwangwali, aliua, alipora na kushambulia na kutesa raia. Ushahidi wa uhalifu huu siyo bayana tu kwa ushiriki wake kwenye uhalifu aliofanya, bali pia unamwajibisha kwa uhalifu uliotendwa na wasaidizi wake.”

Kama hiyo haitoshi..

(Sauti ya Nicole)

“Mtasikia kuhusu watoto kutumwa vijijini kwa ajili ya uporaji. Mtasikia kuwa Bosco Ntaganda mwenyewe alitumia watoto wa umri wa chini ya miaka 15 kama walinzi wake.”

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho ambapo mwakilishi wa wahanga wa uhalifu huo atasoma taarifa yake na hatimaye Bosco Ntaganda atazungumza mwishoni.