Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa kukabiliana na homa ya ini kufanyika Scotland

Mkutano wa kukabiliana na homa ya ini kufanyika Scotland

Zaidi ya nchi 60 zinakutana mjini Glasgow nchini Scotland kuweka mikakati ya kukabiliana na homa ya ini au Hepatitis ambayo ni tishio kwa nchi zenye kipato cha chini na kati.

Mkutano huu wa aina yake unalenga kuokoa maisha ya watu milioni 1.4 wanaokufa kwa ugonjwa huo kila mwaka na unaongozwa na kauli mbiu “wito wa kuzinduka”

Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni WHO, Homa ya ini ambayo huathiri zaidi nchi masikini hususani Hepatitis B na C husababisha asilimia 80 ya vifo vitokanavyo na saratani ya ini huku watu wengi wanaoishi na virusi sugu hawatambui kuhusu maambukizo hayo.

Katika nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara na Asia Mashariki takribani aislimia 10 ya watu wameathiriwa na Hepatitis B sugu. Mkutano huo utafanyika kwa siku tatu ambapo  WHO kwa kushirikiana na shirika la kukabiliana na Hepatitis linataka nchi kukuza mikakati bora dhidi ya ugonjwa huo.