Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanawake na watoto wanaoingia Macedonia yaongezeka

Idadi ya wanawake na watoto wanaoingia Macedonia yaongezeka

Idadi ya wanawake na watoto wanaokimbia ghasia kwenye zao na kuvuka mpaka kuingia Macedonia kusaka hifadhi Ulaya imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ambalo limesema takribani watu Elfu Tatu wanakuwa kwenye vituo vya mpito cha Macedonia kila siku.

UNICEF imesema theluthi moja ya watu hao ni wanawake na watoto ambapo asilimia 12 ni wanawake wajawazito.

Wizara ya ndani ya jamhuri hiyo ya zamani ya Yugoslavia imesema asilimia 80 wanatoka Syria ilihali asilimia Tano ni Afghanistan na tano Iraq.

Wadau wa kibinadamu sasa wanahaha kuwasaidia ambapo UNICEF imepeleka maboza ya maji na mahema na imesisitiza umuhimu wa watoto kulindwa bila kujali hadhi yao.