Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Zeid kuzuru CAR Septemba 1-4, 2015

Kamishna Zeid kuzuru CAR Septemba 1-4, 2015

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameanza leo Jumanne ziara ya siku nne nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako atatathmini juhudi za kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu, na kuhakikisha hatua mathubuti zinachukuliwa mara moja na ipasavyo, kila ukiukaji kama huo unapotekelezwa na vikosi vya kimataifa. Taarifa kamili na Joshua Mmali

Taarifa ya Joshua

Katika ziara yake hiyo, Kamishna Zeid anatarajiwa kukutana na rais wa serikali ya mpito, Catherine Samba-Panza, na viongozi wengine serikalini. Atakutana pia na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu, Kamanda wa vikosi vya kulinda amani vya MINUSCA, makamanda vikosi vya kimataifa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, viongoizi wa kidini, vyama vya kisiasa na wanadiplomasia.

Kamishna Zeid atafanya pia mazungumzo na viongozi wa mikoa, makundi ya vijana na wanawake, na wawakilishi wa wakimbizi wa ndani 368,000.

Aidha, Kamishna Zeid atahutubia mkutano wa kimataifa kuhusu kupambana na ukwepaji sharia, ambao umeandaliwa kwa pamoja na MINUSCA na Ofisi ya Haki za Binadamu, na kutoa wito wa kuhakikisha uwajibishaji kwa ukikuaji wote wa haki za binadamu, na kuhakikisha haki inatendeka kwa waathiriwa wa uhalifu uliotendwa nchini CAR, hususan kupitia kuanzishwa haraka mahakama maalum ya uhalifu.