Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa kigeni waanza kuhamishwa kutoka vituo vya UNMISS vya ulinzi wa raia

Raia wa kigeni waanza kuhamishwa kutoka vituo vya UNMISS vya ulinzi wa raia

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, umetangaza kuanza zoezi la kuwahamisha raia wa kigeni 510 ambao wamekuwa wakiishi katika kituo kimoja cha UNMISS cha ulinzi wa raia karibu na barabara ya Yei mjini Juba.

Zoezi hilo lilianza mnamo Agosti 27 kwa kuwahamishia raia 97 wa kigeni kwenye mji wa Juba, na wengine 16 mnamo Ijumaa Agosti 18.

Zoezi hilo la kuwahamisha raia wa kigeni linatekelezwa na UNMISS, ikishirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM.

Kuzuka kwa mapigano nchini Sudan Kusini mnamo Disemba 2013 kulisababisha mmiminiko wa mamia ya raia wa kigeni kwenye vituo vya ulinzi wa raia vinavyoendeshwa na UNMISS katika siku za kwanza za mapigano. Wengi wao ni raia wa Ethiopia, Eritrea na Somalia.

Taarifa ya UNMISS imesema hali ya usalama imebadilika, na hivyo hakuna haja ya raia hao wa kigeni kuendelea kuishi katika kambi za UNMISS.