UNESCO yalaani mauaji ya mwanahabari Paulo Machava wa Msumbiji
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova, leo ametoa wito kwa serikali ya Musumbiji kufanya uchunguzi katika mauaji ya mwanahabari wa tovuti ya habari ya Diairio de Noticias, Paulo Machava, ambayo yalitokea nchini humo, mjini Maputo.
Akitoa wito kwa mamlaka za Musumbiji kubainisha kiini cha uhalifu huo, Bi Bokova amekaani mauaji ya mwanahabari huyo, akiongeza kuwa bunduki zisitumiwe kunyamazisha vyombo vya habari na kuwanyima watu haki ya kupokea habari kutoka vyanzo mbali mbali.
Paulo Machava, ambaye alikuwa mhariri na mwandishi mkuu wa tovuti ya habari ya Diario de Noticias, alipigwa risasi mnamo Agosti 28 na watu wasojulikana.
Marehemu Machava aliwahi kufanya kazi na radio ya kitaifa ya Rádio Moçambique na jarida la kila wiki la Savana.