Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya Haki za Binadamu yasikitishwa na kurejeshwa adhabu ya kifo Chad

Ofisi ya Haki za Binadamu yasikitishwa na kurejeshwa adhabu ya kifo Chad

Ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, OHCHR, imeeleza kusikitishwa na kurejeshwa kwa adhabu ya kifo nchini Chad.Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Mnamo Jumamosi Agosti 29, watu kumi nchini humo waliuawa kwa kufyatuliwa risasi, baada ya kupewa hukumu ya kifo mnamo Ijumaa, chini ya sheria mpya ya kupambana na ugaidi.

Hii ni mara ya kwanza adhabu ya kifo kutekelezwa nchini humo tangu mwaka 2003.

Ofisi hiyo imeeleza kusikitishwa hasa kwa sababu mnamo Septemba mwaka 2014, serikali ya Chad ilitangaza kuwa sharia mpya ya kupiga marufuku adhabu ya kifo ilikuwa imepitishwa na baraza la mawaziri, lakini bunge la kitaifa likapitisha sharia mpya kuhusu ugaidi mnamo Julai 30 2015, ambayo inajumuisha adhabu ya kifo.

“Matumizi ya adhabu ya kifo ni tukio la kusikitisha, na yanakiuka mapendekezo ya kupiga marufuku adhabu ya kifo, ambayo yaliridhiwa na Chad wakati wa ukaguzi wa mara kwa mara katika Baraza la Haki za Binadamu mnamo Machi 2014. Tunatoa wito kwa serikali ya Chad iweke sitisho rasmi linalolenga kupiga marufuku adhabu ya kifo.”