Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watiwa hofu na ongezeko kubwa la wahanga wa kiraia Yemen

UM watiwa hofu na ongezeko kubwa la wahanga wa kiraia Yemen

Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, imeeleza kutiwa hofu na ongezeko kubwa la idadi ya wahanga wa kiraia huko Taiz, nchini Yemen, katika wiki chache zilizopita.

Aidha, ofisi hiyo imesema inasikitishwa na hali ya tete ya kibinadamu, ambayo inazoroteshwa hata zaidi na kufungwa kwa barabara za kupitisha misaada ya kibinadamu na kamati zinazoegemea upande wa kundi la Houthi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na ofisi hiyo, takriban raia 95 wameuawa katika wiki mbili zilizopita, huku 129 wakijeruhiwa mjini Taiz. Vifo 53 kati ya hivyo 95 vilitokea mnamo Agosti 20 pekee, vikiripotiwa kusababishwa na mashambulizi ya angani ya vikosi vya muungano unaoongozwa na Saudia. Cecile Pouly ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva.

(Sauti ya Cecile)

“Tangu kuongezeka mapigano ya silaha mnamo Machi 26 hadi Agosti 27, raia 2,112 wameuawa nchini Yemen, huku 4,519 wakijeruhiwa. Idadi hii ni makadirio yanayotokana tu na waangalizi wetu kwenye maeneo ya matukio, na idadi kamili huenda ikawa juu zaidi. Tunatiwa wasiwasi pia na athari za kibinadamu zitokanazo na mashambulizi dhidi ya bandari ya Hodeidah, ambayo sehemu muhimu ya kuingiza misaada ya kibinadamu na bidhaa za biashara nchini Yemen.”