Skip to main content

FAO na We Effect kuchagiza maendeleo ya wakulima

FAO na We Effect kuchagiza maendeleo ya wakulima

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kwa ushirikiano na taasisi ya ushirikiano wa maendeleo ya nchini Sweden wamekubaliana kufanya kazi pamoja kuimarisha na vikundi vidogo vya ushirika wa wazalishaji wa mazao ya misitu na mashambani katika nchi zinazoendelea.

Ubia na taasisi hiyo We Effect huo umetiwa saini leo huko Roma, Italia na utaanza kwa kushirikisha nchi Nane zikiwemo Kenya, Malawi na Zambia kwa kipindi cha miaka mitatu.

Akizungumza baada ya utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva amesema ushirikiano huo utawezesha wanachama wa vikundi husika kumiliki ardhi na kupata masoko na hivyo kuinua vipato vyao na vya jamii zao.

Amesema kwa sasa licha ya kwamba sekta ya misitu ni fursa ya ajira kwa watu zaidi ya Milioni 50, wengi wanashindwa kutumia ipasavyo kutokana na kukosa umiliki na hata stadi za kuboresha matumizi ya rasilimali hizo.

Mkuu huyo wa FAO ameongeza kuwa vyama vya ushirika na vikundi vya wazalishaji ni mwelekeo sahihi wa kutokomeza njaa duniani na huwezesha wakazi wa vijijni kufikia masoko na hata kupata majibu ya changamoto kama vile ukosefu wa usawa wa kijinsia.