Zaidi ya watu 800,000 Somalia hawana uhakika wa chakula:FAO

31 Agosti 2015

Utapiamlo uliokithiri unazidi kuenea huko Somalia kutokana na ukosefu wa uhakika wa chakula na hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi hadi mwezi Disemba mwaka huu na kuathiri zaidi ya watu Laki Nane.

Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO likitupia lawama mavuno kiduchu ya nafaka kwenye maeneo ya kilimo, sanjari na mvua ambazo hazikutosheleza na kukwama kwa biashara kutokana na mashambulizi yanayofanywa na vikundi vilivyojihami maeneo ya kusini.

Taarifa ya FAO inasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi wakati wa msimu wa mvua kubwa ambazo hunyesha kati ya mwezi Oktoba na Disemba na hivyo misaada ya dharura ya kibinadamu ikiwemo lishe na afya inahitajika kati ya sasa na mwezi Disemba.

FAO inakadiria kuwa watoto zaidi ya Laki Mbili wenye umri wa chini ya miaka mitano wana utapiamlo uliokithiri na idadi inatarajiwa kuongezeka hadi zadi ya Laki Tatu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter