Skip to main content

Ban afunguka kufuatia kugunduliwa maiti za wakimbizi kwenye lori Ulaya

Ban afunguka kufuatia kugunduliwa maiti za wakimbizi kwenye lori Ulaya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ameeleza kushtushwa na kuvunjwa moyo na majanga ya hivi karibuni ya wakimbizi na wahamiaji kufariki dunia kwenye Bahari ya Mediterenia na Ulaya.

Bwana Ban amesema hayo kufuatia kugunduliwa kwa zaidi ya miili 70 ya watu waliofariki dunia katika lori kwenye mpaka wa Austria na Hungary. Ripoti zinasema kuwa wengi wa wahanga walikuwa raia wa Syria wanaotafuta hifadhi, wakiwemo watoto.

Ban amesema siku za hivi karibuni zimeshuhudia habari zaidi za mamia ya wakimbizi na wahamiaji wakizama kwenye safari hatarishi baharini, akiongeza kuwa licha ya juhudi za pamoja Ulaya za kuwasaka na kuwanusuru waathiriwa, Bahari ya Mediterenia imeendelea kuwa mtego wa kifo cha wakimbizi na wahamiaji.

Katibu Mkuu amesema majanga haya ya mara kwa mara yanabainisha unyama wa wasafirishaji haramu wa binadamu na walanguzi, ambao vitendo vyao vya kihalifu vimeenea kutoka Bahari ya Andaman hadi Mediterenia na hadi barabara za Ulaya, na pia yanaonyesha hali ya kukata tamaa ya watu wanaotafuta maisha bora na usalama. Ameongeza kuwa idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji ni dalili ya matatizo makubwa zaidi- migogoro isiyoisha, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, kufeli kwa utawala na unyanyasaji mkubwa. Muda mfupi baadaye, Katibu Mkuu amerekodi ujumbe wake

“Ni lazima tuelewe ni kwa nini watu wanahatarisha maisha yao. Wanakimbia vita, misukosuko ya kisiasa, na pasipo usalama, kutafuta mustakhbali bora. La kipaumbele kwetu linapaswa kuwa kunusuru maisha na kutoa usaidizi wa kibinadamu. Natoa wito kwa serikali zote kupanua njia za kisheria za uhamiaji, na kufanya vitendo vya kibinadamu, fadhila, na  kulingana na wajibu wao kimataifa.”

Ban amesema, mbali na kutimiza wajibu wake, jamii ya kimataifa inapaswa kuonyesha ari kubwa zaidi ya kutatua mizozo na matatizo mengine yanayowalazimu watu kukimbia makwao, na kwamba ikishindwa kufanya hivyo, idadi ya wanaokimbia ambayo sasa ni 40,000 kwa siku, itazidi kupanda tu.

“Hili ni janga la kibinadamu linalohitaji jitihada za pamoja kisiasa za kujitoa. Ni janga la mshikamano, sio la idadi. Tufanye kila tuwezalo kuwapa watu walioko katika hali mbaya sana usalama na kitu cha kutumainia.”