Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azitaka Colombia na Venezuela zishirikiane kushughulikia hali mpakani

Ban azitaka Colombia na Venezuela zishirikiane kushughulikia hali mpakani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema kuwa anafahamu kilichotokea hivi karibuni katika sehemu kadhaa karibu na mpaka wa Colombia na Venezuela, na hatua nzuri iliyochukuliwa ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje Agosti 26, na ahadi za nchi hizo mbili kuimarisha ushirikiano wao ili kushughulikia changamoto zilizopo.

Mapema Ijumaa, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, ilieleza kutiwa wasiwasi na hali kwenye mpaka wa Colombia na Venezuela, hususan kutokana na ripoti za ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika katika muktadha wa kuwarejesha raia wa Colombia nyumbani.

Ravina Shamdasani ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva..

“Tunatoa wito kwa mamlaka za nchi zote mbili kuhakikisha hali inapatiwa suluhu kupitia majadiliano na mazungumzo, kulingana na wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na sheria ya kimataifa kuhusu wakimbizi. Tunatoa wito kwa mamlaka za Venezuela kuhakikisha kuwa haki za binadamu za waathiriwa wote zinaheshimiwa , hususan katika muktadha wa kuwarejesha wagenu.”