Maiti zapatikana kwenye lori mpakani wahamiaji wanapomiminika Hungary

28 Agosti 2015

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limeeleza kushtushwa na kuhuzunishwa na kupatikana kwa miili ya watu wapatao 70 ndani ya lori lililoegeshwa karibu na mpaka wa Austria na Hungary.

Polisi wa Austria wamesema wanaamini kuwa lori hilo lilitokea Hungary mnamo Jumatano usiku au Alhamis alfajiri, na kwamba wahanga huenda walikuwa wamefariki dunia siku moja au mbili zilizopita.

UNHCR imesema watu hawajatambulika bado, ingawa kuna uwezekano kuwa walikuwa wanasafirishwa na wasafirishaji haramu wa binadamu.

UNHCR imesema janga hilo linadhihirisha ukatili wa wasafirishaji haramu wa binadamu, ambao sasa wamepanua biashara yao kutoka Bahari ya Mediterenia hadi kwenye barabara za Ulaya, huku ikitoa wito kwa nchi za Ulaya zifungue fursa kwa wasaka hifadhi kuingia Ulaya kwa njia za kisheria, ili waepushwe na safari hatarishi zinazoendeshwa na wasafirishaji haramu.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter