Ban awasihi Warundi wadumishe moyo wa makubaliano ya Arusha

28 Agosti 2015

Wakati Burundi ikiadhimisha leo miaka 15 tangu kusainiwa kwanza makubaliano ya amani na maridhiano mjini Arusha, Tanzania, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ametoa wito kwa Warundi wadumishe moyo wa makubaliano hayo wa mazungumzo, uelewano na utatuaji wa mizozo kwa njia ya amani.

Bwana Ban amesema, mchakato wa amani na maridhiano wa Arusha uliweka mazingira ya kuwa na kizazi cha kwanza cha Warundi ambao hawajawahi kushuhudia vita tangu uhuru wa nchi hiyo.

Taarifa ya ofisi ya msemaji wake imemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa mchakato huo wa Arusha umekabiliwa na mtihani mkubwa katika miezi mitano iliyopita.

Ametoa wito kwa viongozi kutoka pande zote kisiasa kuonyesha ujasiri na busara na kurejelea mazungumzo na wakinzani wao, na kuwa na mtazamo unaozidi tofauti zao kisiasa. Aidha, Ban amesema licha ya tofauti hizo kuonekana kuwa kubwa sana, ni ndogo zaidi kuliko gharama ya kurejelea machafuko.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter