Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa zaidi ya 400 vya kipindupindu vyaripotiwa Tanzania- WHO

Visa zaidi ya 400 vya kipindupindu vyaripotiwa Tanzania- WHO

Shirika la Afya duniani(WHO) limesema visa vipya 404 vya kipindupindu vimegunduliwa nchini Tanzania, na kusababisha vifo vya watu wanane katika miji ya Dar-es-salaam na Morogoro, kati ya tarehe 15 na 27 mwezi huu wa watotoAgosti. Taarifa ya Amina Hassan inafafanua zaidi.

(TAARIFA YA AMINA)

WHO imesema, mji mkuu wa Dar-es-salaam ndio uliothirika zaidi, ambapo kumerekodiwa visa 354 vya maambukizi na vifo 7, ikiongeza kuwa mlipuko wa kipindupindu wa kati ya mwezi Mei na Julai  wakati wakimbizi kutoka Burundi walipofurika katika wilaya Kigoma ulidhibitiwa. WHO imesema hakuna kisa kingine kilichoripotiwa miongoni mwa wakimbizi hao mpaka sasa, na kwamba mlipuko huu mpya haujasabishwa na mlipuko wa awali wa Kigoma kwani kuna umbali wa karibu kilomita 1000 kati ya miji hiyo miwili. Christian Lindmeier ni msemaji wa WHO.

(Sauti ya Lindmeier)

“Mlipuko huu sio wa kawaida kwa sasa kwa sababu umezuka kwa haraka kutoka visa mia moja na kupanda hadi visa mia nne na nne, ingawa kipindupindu kinalipuka mara kwa mara Tanzania. Na kwa hivyo siyo kitu cha kutia wasi wasi , lakini ni lazima kishughulikiwe”