Skip to main content

UNHCR yakaribisha makubaliano Sudan Kusini, idadi ya wakimbizi ikiongezeka

UNHCR yakaribisha makubaliano Sudan Kusini, idadi ya wakimbizi ikiongezeka

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limekaribisha kutiwa saini kwa makubaliano ya amani huko Sudan Kusini wakati huu ambapo idadi ya wakimbizi wa ndani imevuka Milioni Mbili nukta Sita, kiwango kilichoripotiwa wakati wa sherehe za uhuru wa nchi hiyo mwezi uliopita.

Msemaji wa UNHCR Geneva, Melissa Flemming amewaeleza waandishi wa habari kuwa idadi ya wakimbizi wa ndani inaongezeka kila uchao hasa Ethiopia ambapo kila siku watu 200 wanasajiliwa ilhali katika nchi nyingine zinazowapokea kama vile Sudan, msimu wa mvua umepunguza idadi ya wakimbizi wapya wanaowasili mwezi huu wa Agosti ikilinganishwa na mwezi Juni na Julai.

Hata hivyo amesema Sudan ilipokea wakimbizi wengi wapya robo hii ya mwaka kutoka Sudan Kusini ikiwa ni ongezeko la asilimia 47.

Bi. Flemming amesema takribani wakimbizi Elfu Nne wa Sudan Kusini wameripotiwa kukimbia makwao huko miji ya Nyongwa, Kerepi na Pageri kwenye jimbo la Equatoria mashariki kutokana na mapigano ya karibuni kati ya vikosi vya serikali na waasi.

Wengi wamesaka hifadhi maporini ilhali wengine wamekimbilia Uganda.