Naibu Mkuu wa OCHA kuzuru DRC kuanzia Jumatatu

28 Agosti 2015

Naibu Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Kyung-wha Kang, Jumatatu anaanza ziara ya siku tano huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yenye lengo la kusaka suluhu la madhila yanayokumba wananchi wa mashariki mwa nchi hiyo. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Msemaji wa ofisi hiyo ya misaada ya kibinadamu, OCHA, Jens Learke ameeleza kuwa ziara itaanzia mji mkuu Kinshasa na kuelekea majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini ambako kwa miaka kadhaa sasa vitendo vya vikundi vilivyojihami vya kutesa raia vimechochea mamia ya maelfu ya wananchi kukimbia makazi yao sambamba na wakimbizi wa kigeni wa Burundi walioko kwenye kambi ya Lusenda.

(Sauti ya Jens)

“Baadhi ya changamoto kuu atakazoibua wakati wa ziara yake ni kushindwa kwa watoa misaada kuwafikia wahitaji mashariki mwa nchi hiyo wakati huu ambapo hali ya usalama imezorota, halikadhalika changamoto ya kupata fedha za kutosha kwa ajili ya operesheni za misaada. Ombi la dola Milioni 692 kwa ajili ya usaidizi limefadhiliwa kwa asilimia 45 tu hadi asubuhi hii.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter