Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia ielekeze macho Chad kusaidia hali ya kibinadamu:Lanzer

Dunia ielekeze macho Chad kusaidia hali ya kibinadamu:Lanzer

Mratibu wa masuala ya kibinadamu ukanda wa Sahel Toby Lanzer leo amekamilisha ziara yake ya siku nne nchini Chad hususani ziwa Chad kutathimini madhara ya kibinadamu, katika mzozo unaoendelea katika ziwa la bonde hilo.

Wakati wa ziara yake, Lanzer ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza mchango wake katika kukabiliana na changamoto za mahitaji ya kibinadamu katika nchi hiyo ambayo ni ya saba kwa kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi duniani.

Amesema kutokana na machafuko ya hivi karibuni, robo ya watu nchini Chad wanahitaji misaada ya kibinadamu husuani katika eneo la ziwa Chad na kuongeza kuwa katika majuma ya hivi karibuni ukosefu wa uslama katika ukanda huo ulisababisha watu zaidi ya 40,000 kukimbia kusaka makazi katika maeneo ya bara.

Mratibu huyo wa masuala ya kibinadamu katika ukanda wa Sahel amesema wengi wao walikimbia bila kitu isipokuwa nguo chache. Wengi hawana maji safi na chakula, na wanakabiliwa na hatari ya magonjwa huku wakikosa malazi na hivyo kulala chini ya miti.