Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atoa tamko kuhusu ripoti za kutumiwa silaha za nyuklia Syria

Ban atoa tamko kuhusu ripoti za kutumiwa silaha za nyuklia Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa ripoti zinazoendelea kutolewa kuhusu matumizi ya silaha za kemikali na kemikali za sumu kama silaha nchini Syria zinasikitisha mno.

Taarifa kutoka ofisi ya msemaji wake imesema Bwana Ban amelaani matumizi yoyote ya silaha kama hizo na upande wowote katika mzozo.

Aidha, Katibu Mkuu amekariri azimio nambari 2235 (2015) lililopitishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama mapema mwezi huu, ambalo ni ujumbe wa pamoja wa jamii ya kimataifa kuwa matumizi ya kemikali kama hizo hayatakubalika kamwe, na kwamba yatakuwa na matokeo yake.

Taarifa hiyo pia imesema, jamii ya kimataifa ina jukumu la kuwawajibisha wanaotenda uhalifu huo, na la kuhakikisha kuwa silaha za kemikali daima hazitumiki tena kama chombo cha vita.

Kufuatia azimio nambari 2235, Katibu Mkuu, akishirikiana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kupinga Silaha za Kemikali, OPCW, leo amewasilisha mapendekezo aliyoombwa na Baraza la Usalama, ukiwemo utaratibu wa uchunguzi wa pamoja utakaowekwa kulingana na azimio kuhusu matumizi ya silaha za kemikali, ikiwemo klorini au kemikali nyingine yoyote ya sumu nchini Syria.

Ametoa wito kwa pande zote nchini Syria zishirikiane ipasavyo na utaratibu wa uchunguzi.