Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia katika mji wa Bambari CAR wawatimua maelfu kutoka makwao

Ghasia katika mji wa Bambari CAR wawatimua maelfu kutoka makwao

Ghasia za siku chache zilizopita baina ya wanamgambo wanaokinzana zimewalazimu maelfu ya watu kuhama makwao katika mji wa Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, limesema Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR.

Hali ilianza kutengamaa mnamo Alhamis, lakini wafanyakazi wa UNHCR wamesema hali mjini Bambari bado ni tete, na wanahofu huenda ikazorota tena.

Mwakilishi wa UNHCR CAR, Kouassi Lazare Etien, amesema wanatiwa wasiwasi na kuongezeka kwa machafuko Bambari na athari zake kwa raia, akiongeza kuwa wafanyakazi wa shirika hilo wamesema kuwa watu waliokimbia makwao wana uoga mwingi.

Ameongeza kuwa UNHCR ina wasiwasi pia kuhusu mamia ya wakimbizi wa Sudan Kusini ambao wamenaswa katika kambi ya wakimbizi karibu na mji wa Bambari, wakikabiliwa na hatari ya kuvamiwa.