Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA na Kazakhstan wasaini makubaliano ya kuhifadhi madini ya urani

IAEA na Kazakhstan wasaini makubaliano ya kuhifadhi madini ya urani

Shirika la Kimataifa la Nisshati ya Atomiki, IAEA, limesaini leo makubaliano na Kazakhstan ya kuanzisha benki ya kuhifadhi madini ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango kidogo, LEU.

Benki hiyo itakayowekwa kwenye mji wa Oskemen, itaendeshwa na Kazakhstan, ingawa itakuwa mahali pa akiba ya madini ya urani yenye rutuba ndogo kwa nchi zote wanachama wa IAEA zinazofuzu kutumia madini hayo, na ambazo haziwezi kuyapata kwenye soko la kimataifa la biashara. IAEA imesema benki hiyo ya urani haitavuruga soko la biashara ya urani.

Madini ya urani yenye rutuba ndogo hutumiwa katika kuzalisha nishati ya nyuklia, na benki hiyo itakuwa na akiba ya tani 90 za LEU, ambazo zinaweza kuendesha kinu kidogo cha maji kinachoweza kuzalisha nishati ya kutumika kwa jiji kubwa kwa miaka mitatu.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukiya Amano, amesema anaamini kuwa benki hiyo ya LEU itaendeshwa kwa njia salama, kulingana na viwango vya usalama vya IAEA kuhusu nyuklia.