Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Menejimenti shirikishi ni siri ya mafanikio kwa kampuni moja Colombia: ILO

Menejimenti shirikishi ni siri ya mafanikio kwa kampuni moja Colombia: ILO

Mfumo wa uboreshaji menejimenti za kampuni ndogo na za kati uonaratibiwa na shirika la kazi duniani, ILO umewezesha kampuni moja nchini Colombia kukua kutoka kuajiri wafanyakazi wawili hadi zaidi ya 80 ndani ya kipindi kifupi.

ILO imesema kampuni ya kutengeneza viatu vya watoto nchini Colombia iitwayo Cala Kids ilikuwa imelenga maduka ya mjini Medellin pekee lakini sasa kuongezeka kwa tija tangu kuanza kutekeleza mfumo huo mwaka 2013, kumesababisha kuanza kwa mipango ya kuuza bidhaa zake hadi nchi zingine za Amerika Kusini.

Mfumo huo uitwao SCORE huweka muundo ambamo kwao wafanyakazi wote wanaweza kutoa maoni ya kuboresha kampuni sanjari na kuwepo kwa kikundi maalum cha kujumuisha mawazo mapya ya kuinua tija hasa kwa kampuni ndogo na za kati ambako mazingira ya kazi mara nyingi ni duni.

Mtaalamu mwandamizi wa ILO katika mradi huo kwenye eneo la Andean, Philippe Vanhuynegem, amesema SCORE inalenga kupunguza uhahifu wa bidhaa, ajali kazini, utoro pamoja na gharama huku ikiongeza mashauriano kati ya mwajiri na mwajiriwa.Kwa sasa mfumo wa SCORE unatekelezwa katika nchi Tisa za Afrika, Asia na Amerika Kusini ukihusisha biashara 545 na mafunzo kwa zaidi ya wafanyakazi 155,000.