Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNEP ahitimisha ziara Uganda

Mkuu wa UNEP ahitimisha ziara Uganda

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP Achim Steiner amehitimisha ziara yake nchini Uganda ambayo pamoja na mambo mengine imemwezesha kukabidhi kitabu cha ramani ya maeneo oevu nchini humo. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Taarifa ya UNEP imesema kitabu hicho ni moja ya michango ya uzinduzi wa mkakati mkubwa wa kuboresha maeneo oevu nchini Uganda na kinatokana na tathmini ya miaka 10 kwenye maeneo oevu ya mijini Kampala, Mukono na Wakiso.

Serikali ya Uganda iliomba UNEP kufanya mchakato huo wenye lengo la kuboresha matumizi ya maeneo oevu wakati huu ambapo matumizi yake holela yanachagiza kuzorota kwa tabianchi.

Bwana Steiner amesema Uganda imebarikiwa maliasili nyingi na UNEP iko tayari kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha zinatumika kiendelevu.

Wakati wa ziara hiyo alikuwa na mazungumzo na Rais Yoweri Museveni ambapo walijadili masuala nyeti ya mazingira ikiwemo matumizi ya nishati huishi na shughuli za kiuchumi zinazojali mazingira.