Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango mpya kuchagiza kutokomeza NTDs ifikapo 2020

Mpango mpya kuchagiza kutokomeza NTDs ifikapo 2020

Shirika la afya ulimwenguni, WHO leo limezindua mpango wa kimataifa wa kujumuisha vyema mradi wa maji, afya na usafi wa mazingira , WASH kwenye mikakati mingine minne ya kiafya ili kutokomeza haraka magonjwa yasiyopatiwa kipaumbele, NTDs ifikapo mwaka 2020. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

WHO imesema imechukua hatua hiyo kwa kuwa magonjwa yasiyopatiwa kipaumbele kama vile kichocho na vikope yanakumba mamilioni ya watu duniani hususan watoto ilhali majibu yake yako dhahiri.

Mkurugenzi wa idara ya afya ya umma na mazingira katika WHO Dokta Maria Neira ametaja suluhu hizo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, kudhibiti kinyesi cha binadamu na kuimarisha huduma za kujisafi.

Amesema hatu hizo siyo tu zitaimarisha afya bali pia zitapunguza umaskini ikiwemo kudhibiti magonjwa 16 kati ya 17 ya NTDs.

Ripoti ya hivi karibuni inaonyesha kuwa watu Bilioni Mbili na Nusu hususan katika nchi maskini hawana huduma za kujisafi, kujisaidia hovyo kukiwa kihatarishi cha kusambaza magonjwa yasiyopatiwa kipaumbele ambayo kila mwaka husababisha vifo vya watu karibu Laki Tano.