Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Kiir kwa kusaini makubaliano Sudan Kusini: Ban

Heko Kiir kwa kusaini makubaliano Sudan Kusini: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hatua ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ya kutia saini makubaliano yenye lengo la kupatia suluhu ya mzozo nchini humo.Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akisema kuwa hatua hiyo ni nyeti na muhimu katika kumaliza mzozo wa miezi 20 ambao umesambaratisha Sudan Kusini na kutumbukiza raia wake kwenye machungu yasiyoelezeka.

Amesema kilichosalia sasa ni kwa pande hizo kutekeleza vipengele vya makubaliano hayo kwa nia njema ikiwemo kupatia ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS fursa ya kuwafikia bila vikwazo vyovyote wahitaji wa misaada ya kibinadamu.

Ban amesema anatambua safari ya utekelezaji ina changamoto huku akisema wakati wa mkutano wa 70 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ataitisha kikao cha ngazi ya juu kuhusu Sudan Kusini akitaraji viongozi wa nchi hiyo kushiriki ili kupanga mustakhbali wa taifa hilo changa Zaidi Afrika.

Katibu mkuu pia amepongeza mamlaka ya IGAD kwa juhudi zake za  bila kuchoka katika kusaka suluhu ya mzozo huo ikiwemo kuratibu mazungumzo ambayo amesema yamehitimishwa kwa mafanikio.

Amesema ameguswa na ushirikiano wenye malengo uliodhihirishwa na viongozi wa ukanda huo katika kumaliza mgogoro huo wa kutisha.

Hata hivyo amesema ushirikiano huo unapaswa kuendelea ili kupata Amani ya kudumu Sudan Kusini na kwamba Umoja wa mataifa uko tayari kusaidia pande husika katika makubaliano hayo, sambamba na IGAD na wadau wa kimataifa.