Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Afrika Mashariki zaahidi kuendeleza ushirikiano wa utalii kikanda

Nchi za Afrika Mashariki zaahidi kuendeleza ushirikiano wa utalii kikanda

Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuendeleza ushirikiano zaidi wa kikanda katika sekta ya utalii. Hayo yameibuka kufuatia kongamano la kwanza maendeleo ya utalii Afrika Mashariki, ambalo liliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, UNWTO, kuanzia Agosti 20 hadi 22, 2015.

Kongamano hilo liliwaleta pamoja viongozi wa kikanda wa sekta ya utalii na wadau wengine ili kutafuta fursa za kuboresha maendeleo endelevu ya utalii kupitia ushirikiano wa kikanda.

Katibu Mkuu wa UNWTO, Taleb Rifai, amesema shirika hilo linaendeleza imani yake katika uwezo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuchukua nafasi ya kwanza katika maeneo yanayopendelewa na watalii, kwa kutoa kivutio kimoja thabiti.

Kwa mantiki hiyo, amekaribisha kuanzishwa hivi karibuni kwa visa ya utalii ya Afrika Mashariki, ambayo inawaruhusu wageni kuzuru Kenya, Rwanda na Uganda, kama fursa ya kuchagiza utalii wa kikanda na kutoa fursa kwa watalii kufurahia wingi wa vivutio katika ukanda mzima.