Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yaidhinisha uhakiki na uangalizi wa Iran kutokana na azimio la Baraza la Usalama

IAEA yaidhinisha uhakiki na uangalizi wa Iran kutokana na azimio la Baraza la Usalama

Bodi ya magavana wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA, leo imetoa mamlaka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Yukiya Amano, kutekeleza uhakiki na uangalizi wa ahadi za Iran zinazohusiana na nishati ya nyuklia, chini ya mpango wa pamoja wa kuchukua hatua, JCPOA.

Mpango wa JCPOA uliafikiwa hivi karibuni baina ya Iran na nchi sita, zikiwa ni Marekani, Uchina, Uingereza, Ufaransa, Urusi, Ujerumani pamoja na Muungano.

Bodi hiyo pia imeidhinisha marekebisho ya mpango na bajeti husika ya IAEA, na kukubali kutafuta Euro milioni 9.2 za ziada kwa ajili ya kutekeleza shughuli za IAEA nchini Iran mwaka 2016, kama ilivyopitishwa na Baraza la Usalama.

Huyu hapa ni Bwana Yukiya Amano, akikutana na waandishi wa habari mjini Vienna baada ya mkutano huo wa halmashauri ya magavana wa IAEA.

“Nimefurahishwa kuwa bodi hii imetoa idhini yake. Hili litakuwa moja ya majukumu muhimu zaidi kuwahi kutekelezwa na IAEA. Kutokana na JCPOA, Iran itatekeleza itifaki ya ziada ya kulinda makubaliano yake IAEA. Nakaribisha hatua hii.”

Bwana Amano ameeleza umuhimu wa Iran kutekeleza itifaki hiyo ya ziada..

“Itifaki ya ziada ni chombo cha kuhakiki chenye nguvu, na nimekuwa nikitoa wito kwa Iran kuitekeleza tangu niliposhika usukani miaka sita iliyopita. Itifaki hiyo ya ziada ikishatekelezwa, tutakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kupata taarifa na kufikia vituo vya nyuklia nchini Iran.”