Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kujadili hali nchini Sudan Kusini

Baraza la Usalama lakutana kujadili hali nchini Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na mkutano kuhusu hali nchini Sudan Kusini, na kufanya mashauriano kuhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Mkutano wa Baraza la Usalama leo umehutubiwa na baadhi ya maafisa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, akiwemo Bi Ellen Margrethe Løj, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, ambaye amesema hali ya kibinadamu nchini humo ni mbaya mno..

“Zaidi ya watu milioni 2.2 wamefurushwa makwao. Zaidi ya watu milioni 4.6 tayari wanakabiliwa na mzozo na hali ya dharura ya kutokuwa na uhakika wa chakula. Hali katika jimbo la Unity hasa inatisha, kwani hali mbaya ya usalama inazuia wahudumu wa kibinadamu kuzifikia jamii zilizohama makwao.”

Kuhusu hali ya haki za binadamu, amesema ameshangazwa na jinsi pande kinzani zisivyoheshimu uhai wa mwanadamu.

Akieleza matumaini yake kuwa serikali itasaini mkataba wa Amani, Bi Løj amesema..

“Ningependa kukariri wito wangu kwa viongozi wa Sudan Kusini, kuweka maslahi ya watu wao juu ya tamaa yao binafsi na kutekeleza makubaliano ya amani kwa roho safi.”

Wengine waliohutubu kwenye mkutano huo ni Mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Stephen O’Brien, na Hervé Ladsous, Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa, na Balozi Cristian Barros wa Chile, Mwenyekiti wa Kamati ya Vikwazo ya Baraza la Usalama.