Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawasaidia watoto wanaokimbia machafuko na wanahamia Ulaya

UNICEF yawasaidia watoto wanaokimbia machafuko na wanahamia Ulaya

Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limeweka kituo cha kuwasaidia watoto na timu ya kuhamishika karibu na mji wa Geveglija, karibu na mpaka wa Ugiriki, ili kutoa msaada kwa watoto na wanawake wakimbizi, ambao wapo safarini kupitia Jamhuri ya Yugoslavia ya zamani ya Macedonia.

Kituo hicho kimewekwa kwenye maeneo ya wahamiaji kupumzikia, yaliyowekwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, kuwasaidia watu wanaokimbia machafuko Syria, Iraq na Afghanistan.

Timu za UNICEF zinawasaidia watoto hao kuunganishwa tena na familia zao, na kutoa usaidizi wa kisaikolojia na huduma za malezi kwa watoto. UNICEF imepata pia vifaa vya watoto kutumia kwa kuchora, kucheza na kusoma, na kituo hicho rafiki kwa watoto kinaweza kuhudumia watoto 50 wakati mmoja.

“Kituo hicho kinatoa sehemu salama kwa watoto kupumzika na kucheza, wakati familia zikikamilisha shughuli za kujiandikisha. Halikadhalika, timu ya kuhamishika inakagua na kutambua, na kisha kuwasilisha mbele watoto wanaohitaji huduma maalum za ulinzi.”

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, idadi ya watu wanaokimbia kupitia Macedonia imeongezeka kutoka 1,500 hadi 2,000 kwa siku, asilimia 30 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto.