Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo cha mawasiliano chazinduliwa kurahisisha huduma za kibinadam Iraq

Kituo cha mawasiliano chazinduliwa kurahisisha huduma za kibinadam Iraq

Wakati idadi ya wahamiaji wa ndani inaongezeka kila uchao nchini Iraq, Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamezindua kituo cha mawasiliano ili kurahisisha utoaji wa huduma za kibinadamu kwa maelfu wanaokimbia makwao juu ya mzozo nchini humo. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Uzinduzi huu umefanyika wakati idadi ya waliokimbia makwao tangu mapema mwaka jana ni zaidi ya milioni 3.1 ambapo wamesambaa kwenye sehemu mbali mbali humo, wakihitaji msaada wa kibinadamu kama chakula na dawa.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Iraq Bruno Geddo amesema, uboreshaji huu wa mawasiliano umewalenga zaidi wale wanaoishi nje ya makambi rasmi, wengi wakiwa katika maeneo yasiofikika.

Amesema hiki kitasaidia waathirika kushiriki katika mchakato wa kusambaza misaada ya kibinadamu, kwani mawasiliano sasa ni kutoka pande zote.

Kwa sasa popote alipo mtu nchini Iraq yaweza kupata habari kuhusu huduma za kibinadamu kuanzia saa mbili ya asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, Jumapili hadi Alhamisi kwa kupiga namba ya simu ya 6999.