Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya afya ni tete kambini Yarmouk na jirani: UNRWA

Hali ya afya ni tete kambini Yarmouk na jirani: UNRWA

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limefanikiwa kukusanya taarifa za kiafya za raia walioko katika wilaya iitwayo Yalda iliyoko karibu na kambi ya wakimbizi ya Yarmouk inayoshikiliwa na kundi linalotaka kuweka dola la kiisilamu ISIS nchini Syria.

Taarifa ya UNRWA inasema kuwa imefanya vipimo zaidi ya 500 vya watu ambao wengi wao wametoka kambi hiyo na kubaini visa 23 vya homa ya matumbo kwa kitaalamu typhoid ikiwa ni mara mbili ya idadi ya visa vilivyobaibishwa awali.

Shirika hilo linasema kuwa takwimu hizo ni ongezeko mara tatu la visa vya awali katika ripoti iliyotolewa mnamo Agosti 18.

Kufuatia hali hiyo, UNRWA inasema kuwa hali ya kiafya kwa wakimbizi nchini Syria ni tete hususani kambini kwenyewe ambako hakuna huduma za afya na hivi karibuni maji yalikatwa. Pia shirika hilo limeongeza kuwa kiwango cha nyuzi joto hivi sasa mjini Damascus kinafikia 41°C (105°F) hali ambayo inaongeza wasiwasi wa ukosefu wa maji.