Skip to main content

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Ujumbe wa UM Kosovo, UNMIK

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Ujumbe wa UM Kosovo, UNMIK

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili ujumbe wa umoja huo nchini Kosovo, UNMIK.

Baraza hilo limehutubiwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa UNMIK, Farid Zarif, ambaye ameanza kwa kusifu hatua muhimu iliyochukuwa na taasisi za Kosovo mnamo Agosti 3 mwaka huu, pale bunge lilipofanyia marekebisho katiba na sheria za kuweka Mahakama Maalum na Ofisi Maalum ya Mwendesha Mashtaka.

Amesema kucheleweshwa kwa hatua hiyo kulikuwa kunaibua wasiwasi mkubwa kutoka kwa wadau mbali mbali, kama ilivyodhihirika katika ripoti ya Katibu Mkuu.

Aidha, Bwana Zarif amesema kuwa kuwekwa kikamilifu utawala wa sheria kunakabiliwa na changamoto nyingine muhimu, akitaja baadhi yazo

Moja yake ni ulinzi wa maeneo ya urithi wa kitamaduni na kidini kisheria. Kuheshimu, kulinda na kutunza urithi wa kitamaduni wa KiOrthodox wa Serbia ni majukumu muhimu, na pia mtihani kwa taasisi za utawala za Kosovo. Zikishindwa kutimiza haya, majukumu na wajibu mwingine muhimu huenda ukawa hatarini.”

Kadhalika, Bwana Zarif amesema hali Kosovo imebadilika sasa, ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka minne iliyopita.

Nilipowasili Kosovo, punde baada ya matukio yam waka 2011, hali ilikuwa tete sana. Barabara zilikuwa zimefungwa kaskazini, na vikosi vya usalama vya kimataifa vilikuwa vimelazimika kuchukua nafasi za kuzuia hali kuzorota. Uhasama wa kisiasa ulikuwa umetanda baina ya Belgrade na Pristina, na ujumbe wa maridhiano ulikuwa haba kutoka pande zote. Miaka minne baadaye, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.”

Amesema sasa Waserbia wa Kosovo wanashiriki uchaguzi na kuchaguliwa kuwakilisha katika nyadhfa za ubunge na uwaziri, na pia hatua zimechukuliwa kuimarisha mfumo wa sheria.