Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yalaani unyanyasaji wa kingono CAR

MINUSCA yalaani unyanyasaji wa kingono CAR

Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, Diane Corner, amelaani vitendo vyote vya ukatili wa kingono vilivyofanywa na askari wa MINUSCA.

Akiwahutubia waandishi wa habari mjini New York kupitia njia ya video, Bi Corner ameelezea ari ya ujumbe huo kupatia suluhu tatizo hilo, na kuhakikisha kuwa MINUSCA inatimiza wajibu wa mamlaka yake, kuwahudumia watu wa CAR, wakiwemo waathiriwa wa vitendo kama hivyo vya unyanyasaji.

Aidha, amesema kuwa kwa ujumla, vimerekodiwa visa 13 vya unyanyasaji wa kingono ambavyo vinadaiwa kuwahusisha askari wa MINUSCA tangu Septemba 14, 2014, tisa kati ya hivyo vikihusu watoto.

“Kuongezeka kasi kwa visa vilivyoripotiwa katika miezi mitatu kunasikitisha. Unyanyasaji wa kingono ni tatizo kubwa mno, na ambalo tumejitoa kutokomeza. Kuwalinda raia jambo la kipaumbele katika mamlaka yetu, na tunalipa jukumu hilo uzito.”