Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa UM asikitishwa na athari za mzozo Yemen kwa raia

Mratibu wa UM asikitishwa na athari za mzozo Yemen kwa raia

Mratibu wa masuala ya kibinadamu Yemen, Johannes Van Der Klaauw, ameeleza kusikitishwa na athari kubwa za mzozo wa Yemen dhidi ya raia nchini humo.  Kufikia sasa, watu wapatao 4,500 wameuawa, na 23,000 wengine kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni raia.

Amesema pia imeshuhudiwa hali ya raia kutoweza kupata huduma muhimu na bidhaa za kuokoa maisha, mzozo huo unapoendelea kufukuta.

Bwana Van Der Klaauw amesema raia sio tu wanakumbwa na vitendo vya kikatili, kama ilivyoonekana Aden na Taizz, lakini pia miundombinu ya kiraia ambayo ni muhimu kwa utoaji wa huduma muhimu na kwa sekta ya biashara, inaharibiwa na pande zote  katika mzozo.

Amesema kulenga na kuharibu miundombinu muhimu ya kiraia ni lazima kukome, na kutoa wito kwa pande kinzani kufanya mazungumzo ya kisiasa ili kukomesha vita na taabu ya raia.