Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahaha kutoa huduma za dharura kwa wakimbizi wa Sudan Kusini

WHO yahaha kutoa huduma za dharura kwa wakimbizi wa Sudan Kusini

Shirika la Afya Duniani, WHO, na wadau wanahaha kukabiliana na mahitaji ya maelfu ya wakimbizi wa ndani kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, ambako mapigano yanaendelea, huku hali ya kibinadamu ikisalia kuwa tete.

Zaidi ya watu 10,000 wamewasili kwenye kituo cha ulinzi wa raia cha Malakal tangu Agosti mosi 2015, kutokana na eneo hilo kutengwa na huduma zote. Mmiminiko huo mpya wa wakimbizi unafanya idadi nzima ya wakimbizi wa ndani kwenye kituo hicho kuwa 46,567, huku familia zikisongamana, bila maji safi au huduma za kujisafi.

Dkt. Allan Mpairwe, ambaye ni Mkuu wa WHO wa Milipuko na Udhibiti wa Majanga Sudan Kusini, amesema kuwa kusongamana kwa wakimbizi husababisha uchafuzi wa maji na magonjwa kama ya kuhara, hepatitis E na kipindupindu.

Kutokana na udharura wa mahitaji ya wakimbizi hao, WHO imesema kuna haja ya kuimarisha utaratibu wa kuratibu na kuongeza huduma za afya, upatikanaji wa maji safi na huduma za kujisafi. Mbali na kipindupindu na magonjwa mengine ya maji, malaria, surua na polio ni miongoni mwa hatari nyingine za kiafya kwa wakimbizi hao wa ndani.