Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jengeni utu ili kutoa misaada ya kibinadamu:Ban

Jengeni utu ili kutoa misaada ya kibinadamu:Ban

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa Ban Ki-moon, amesema kila mmoja wetu ana uwezo na wajibu wa kusaidia kujenga ulimwengu wenye utu wema zaidi, akitoa wito kwa kila mtu kujiunga kwenye kampeni ya ShareHumanity. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Umoja wa Mataifa umetenga siku hii kwa ajili ya wahanga wa shambulizi la Baghdad lililokatili maisha ya watu 22, akiwemo aliyekuwa mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, Sergio Vieira de Mello.

Katika Ujumbe wake, katibu mkuu Ban Ki-moon amesema siku hii ni ya kuwaenzi watu wanaojitolea kibinafsi, bila kujijali, katika mazingira hatarishi ili kuwasaidia wenzao wanaoishi katika hali ngumu.

Sauti ya Ban

“Najua wote mna uchungu kama mimi na mateso katika maeneo mengi duniani. Kutojali miongoni mwa wale wenye uwezo wa kuleta mabadiliko kunawaacha watu wengi mno bila matumaini. Katika siku hii nawasihi watu wote kuonyesha mshikamano kama raia wa kimataifa kujisajili katika kampeni iitwayo ShirikiUbinadamu ama ShareHumanity”

Zaidi ya watu nusu milioni wamekuwa wakiweka hadithi za manusura wa mizozo ya kibinadamu kwenye kurasa zao za Facebook na Twitter, kama sehemu ya kampeni ya dijitali iliyozinduliwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake wiki iliyopita, kwa ajili ya kuhamasisha ubinadamu.