Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Yemen umewaacha maelfu ya watoto wahanga: UNICEF

Mzozo wa Yemen umewaacha maelfu ya watoto wahanga: UNICEF

Wastani wa watoto wanane wanauawa au kulemazwa kila siku nchini Yemen kutokana na mzozo unaoikumba nchi hiyo. Hii ni kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

Ripoti hiyo iitwayo, Yemen: Utoto mashakaniinasema kwamba takriban watoto 400 wameuwawa na zaidi ya watoto 600 kujeruhiwa tangu kuongezeka kwa ukatili miezi minne iliyopita.

UNICEF imesema kwamba kukatizwa kwa huduma za afya, kuongezeka kwa visa vya utapiamlo, kufungwa kwa shule na idadi kubwa ya watoto wanoingizwa katika vikundi vya vita ni miongoni mwa athari za mzozo wa Yemen.

Kadhalika UNICEF imesema kwamba watoto wanauwawa kwa bomu na risasi huku wanaonusurika wakikabiliwa na magonjwa na utapiamlo. Simon Ingram ni msemaji wa UNICEF

“Mmoja wa watoto tuliyezungumza naye ni msichana wa miaka tisa kwa jina, Latifa. Alieleza jinsi alivyokuwa nje na dada zake wakati mabomu yalikuwa yakilipuka kandoni mwao. Alisema kwamba illikuwa vigumu kuwaona kwa sababu ya vumbi iliyowazingira, na ilikuwa vigumu kupumua. Aidha alieleza alivyoogopa na kuomba apate ulinzi.”

Ripoti hiyo imetaja madhila yanayosababishwa na mzozo kwa maisha ya watoto sasa hivi na matokeo yake kwa mustakhabali wao.