Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel itimize wajibu kuimarisha uchumi na biashara maeneo yaliyokaliwa Palestina: UNCTAD

Israel itimize wajibu kuimarisha uchumi na biashara maeneo yaliyokaliwa Palestina: UNCTAD

Palestina huenda ikaimarisha sekta yake ya biashara iwapo Israeli itatimiza wajibu wake kisheria chini ya makubaliano ya Shirika la biashara duniani WTO kuhusu kuwezesha biashara katika maeneo yaliyokaliwa ya Palestina. Hii ni kulingana na ripoti ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo, UNCTAD.

Ripoti hiyo yenye jina “Makubaliano ya mwaka 2013 ya Shirika la biashara duniani na uwezeshaji wa biashara: Wajibu wa Israeli kuhusu biashara Palestina", ni makubaliano yaliyoafikiwa Bali, Indonesia mwaka 2013 kwa lengo la kuondoa vizuizi na kuimarisha usafirishaji wa bidhaa mipakani na kutozwa kwa ushuru na wanachama wote wa WTO na maeneo wanakosimamia.

Kukaliwa kwa maeneo ya Palestina kwa muda mrefu, kumesababisha Palestina kupoteza usimamizi wa mifumo mbali mbali ya biashara na kwa sasa inakabiliwa na ubaguzi kama vile vyeti vinavyohitajika na vikwazo vya uagizaji wa bidhaa chini ya mfumo wa Israeli. Hali ambayo imesababisha umasikini, ukosefu wa uhakika wa chakula na idadi kubwa ya ukosefu wa ajira.

Matthew Brown ni msemaji wa UNCTAD

Utafiti huu umebaini kwamba Israeli kama mwanachama wa WTO na mamalaka inayokalia Palestina ina wajibu mkubwa juu ya Palestina, kusaidia Palestina kwenye mfumo ulio wazi na wa haraka wa ushuru, kupunguza nyaraka zinazohitajika na muda wa utaratibu huo kuvuka mipaka.”

Ameongeza kwamba hatua hii iwapo itachukuliwa, itasaidia kuimarisha hali ikiwemo kuongeza ajira ambayo kulingana na takwimu za mwaka 2014 ilifikia asilimia 44%.